SHEIKH JALALA ATOA WITO WA KUKITHIRISHA TAQ'WA ILI KUZUIA UFISADI
Dar es Salaam - Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna'asharia Tanzania (T.I.C Taifa), Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, amesisitiza umuhimu wa kuwa na Khofu ya Mwenyezi Mungu (SWT) na kukinai neema alizoruzukiwa mwanadamu kama njia ya kuzuia ufisadi na uharibifu katika jamii.
Akihutubu leo Tarehe 7/6/2025 sawa na Tarehe 10 DhulHijjah Mwaka 1446 katika Khutba ya Swala ya Eid al-Adh'ha iliyofanyika katika Masjid Ghadir, Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mwakindenge amesema kuwa mtu mwenye taq'wa huwa na moyo wa kuridhika hata na kidogo, hali ambayo humkinga dhidi ya tamaa na uovu.
"Mtu mwenye Khofu ya Mungu ndani yake huwa na kukinai; lakini kukosekana kwa hali hiyo ya kuridhika kunapelekea matendo ya ufisadi na uharibifu," amesema Sheikh Mwakindenge katika khutba hiyo iliyobeba kichwa cha habari "Umuhimu wa Taq'wa Katika Masiku Haya."
Aidha, Sheikh Mwakindenge amewataka waumini kutumia siku hizi tukufu za Hija kwa kutafakari kwa kina kuhusu nafasi ya maadili, uadilifu, na uchamungu katika maisha yao ya kila siku.
Maadhimisho ya Eid al-Adh'ha yamefanyika kwa amani huku waumini kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wakijumuika kwa ibada, dua na sadaka, kuenzi tukio la kujitolea kwa Mtume Ibrahim (AS).








