Breaking News

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AONGOZA JUKWAA LA VIJANA NA MAZINGIRA

Dar es salaam -Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameshiriki kama mgeni rasmi katika Jukwaa la Vijana na Mazingira lililofanyika leo, Juni 3, 2025, katika ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Jukwaa hilo limekusanya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwaunganisha na kuwajengea uelewa juu ya masuala ya mazingira, sambamba na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kubuni na kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto za kimazingira nchini.

Tukio hilo ni sehemu ya maadhimisho kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, na limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Taasisi ya Africa Carbon Agency.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza umuhimu wa kushirikisha vijana katika juhudi za kutunza mazingira, akieleza kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa na wana nafasi ya kipekee katika kuleta mabadiliko chanya ya kimazingira. Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kuendeleza ubunifu na miradi ya mazingira kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Jukwaa hili limejumuisha mijadala, maonyesho ya miradi ya vijana, na warsha mbalimbali zenye lengo la kuwahamasisha vijana kuchukua hatua katika kulinda mazingira yao kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.