WMA UHAKIKI VIPIMO KILA BAADA YA MIEZI 12 - MAVUNDE
Meneja wa Kituo cha Ukakiki wa Vipimo (WMA) Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani, bwana Charles Mavunde akitoa maelezo kwa mwandishi namna ambavyo kifaa hicho kinafanya kazi
Meneja wa Kituo cha Ukakiki wa Vipimo (WMA) kilichopo Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani Charles Mavunde akielezea namna kituo hich cha Ukakiki wa Vipimo (WMA) kilichopo Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani
Kifaa ambacho hufungwa kwenye mita ambazo zimehakikiwa na WMA.
Kutoka kushoto ni Ofisa Mkuu Vipimo Gaudence Gaspery akitoa maelezo kuhusu mita za DAWASA na kulia ni Meneja wa Kituo cha WMA Kibaha Charles Mavunde.
Pwani — Meneja wa Kituo cha Ukakiki wa Vipimo cha Wakala wa Vipimo (WMA) kilichopo Misugusugu, Kibaha, Charles Mavunde, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340, vipimo vyote vinavyotumika katika biashara na huduma mbalimbali nchini lazima vihakikiwe kila baada ya miezi 12 ili kuhakikisha usahihi wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, bwana Mavunde alibainisha kuwa Sheria hiyo, iliyofanyiwa marekebisho na kuanza kutumika mwaka 2002, kupitia kifungu namba 19, inasisitiza uhakiki wa vipimo vinavyotumika kupima ujazo, urefu na uzito.
“Katika uhakiki huu, Wakala wa Vipimo tunazingatia sheria kwa kuhakikisha vifaa vinavyotumika kupima vinafanyiwa ukaguzi kila baada ya miezi 12. Mtu yeyote atakayeshindwa kufanya hivyo anakabiliwa na adhabu ya faini kati ya Sh. 100,000 hadi Sh. milioni 20 au kifungo cha miaka miwili jela,” alisema Mavunde.
Bwana Mavunde alieleza kuwa wananchi wameonyesha mwamko mkubwa wa kuhakiki dira za maji, na akatoa wito kwao kutoa taarifa wanapohisi kuna dosari katika ankara wanazopata kutoka kwa watoa huduma.
“Uhakiki huu unaendelea. Wananchi washirikiane na WMA. Tunapoona ankara ni kubwa mno, huenda kipimo si sahihi. Tuwe na ushirikiano ili kila mmoja apate haki yake — mtoa huduma na mpokeaji,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Mavunde, faida za kuhakiki vipimo ni pamoja na kuhakikisha mteja analipa kiasi sahihi cha fedha, huku mamlaka husika zikipata makusanyo ya haki kwa mujibu wa matumizi halali.
“Tunafanya uhakiki wa mita za maji, mita za umeme, malori ya mafuta, gesi na vifaa vyote vinavyotumia vipimo katika biashara na huduma. Hili ni muhimu kwa haki ya pande zote mbili,” alisema.
Akitaja hatua zilizochukuliwa, Mavunde alisema kuwa wanatarajia kuhakiki mita za maji zaidi ya 87,000 hadi kufikia mwisho wa Juni 2025, kabla ya kufungwa kwa wateja. Aidha, zaidi ya mita 5,500 za umeme wa viwandani tayari zimehakikiwa.
“Tunafanya uhakiki pia kwa mita za majumbani ili kuhakikisha TANESCO, mamlaka za maji na watumiaji wa mwisho wote wananufaika kwa usahihi wa vipimo,” alisema.
Kuhusu malori ya vimiminika, Mavunde alisema kuwa hadi sasa zaidi ya malori 5,900 yamehakikiwa tangu Julai 2024 hadi Mei 2025, wakivuka lengo. Uhakiki huo hufanyika katika vituo vya Mtwara, Mwanza na Iringa kwa malori ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Ofisa Vipimo Mkuu, Gaudence Gaspery, alisema kuwa kwa sasa wanatumia mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuhakiki mita 10 kwa wakati mmoja.
“Baada ya kuhakikiwa, mita zinazoonekana zinafaa huwekewa rakili ya rangi ya machungwa. Zile zinazohitaji marekebisho hushughulikiwa, na zisizofaa huteketezwa,” alisema Gaspery.
WMA ina uwezo wa kuhakiki mita 100,000 kwa mwaka, na tayari mita 30,000 za DAWASA zimewasilishwa kwa ajili ya uhakiki.








