Breaking News

BRELA WAANDISHI JITOKEZENI KUSHIRIKI TUZO ZA KIKANDA ZA MILIKI UBUNIFU


Dar es Salaam – Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (ARIPO) wamewataka waandishi wa habari nchini kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya kushiriki katika shindano la kikanda la uandishi wa habari kuhusu miliki ubunifu.

Shindano hilo limeandaliwa na ARIPO kwa kushirikiana na mpango wa Innovation for Africa (AfrIPI) na linahusisha waandishi kutoka vyombo vya habari ikiwemo runinga, redio, magazeti na mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa BRELA, lengo la tuzo hizo ni kutambua na kuthamini mchango wa waandishi wanaoibua na kutangaza habari zinazohusu miliki ubunifu, pamoja na wabunifu walioko katika nchi wanachama wa ARIPO, ikiwemo Tanzania.

“Tuzo hii inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu thamani ya ubunifu na namna unavyoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa nchi wanachama,” imeeleza taarifa ya BRELA.

Mashindano haya yanatokana na maazimio ya mkutano mkuu wa ARIPO uliofanyika mwaka 2022/2023. Waandishi wote nchini wanahimizwa kushiriki kwa kuwasilisha kazi zao za uandishi kabla ya tarehe 30 Agosti 2025.

Kazi hizo zinaweza kuwasilishwa katika makao makuu ya BRELA au kwa barua pepe info@brela.go.tz. Kwa maelezo zaidi, waandishi wanashauriwa kupiga simu namba +255 (0) 22 221 2800.