Breaking News

KIGOMA YAONGEZEWA MTANDAO WA BARABARA ZA LAMI KWA ASILIMIA 87.3

MKOA wa Kigoma umeendelea kupata maendeleo makubwa katika sekta ya miundombinu ya barabara chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo mtandao wa barabara za kiwango cha lami umeongezeka kwa asilimia 87.3 ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Takwimu zinaonyesha kuwa, barabara za lami zimeongezeka kutoka kilomita 53.7 mwaka 2020 hadi kilomita 100.7 mwaka 2025. Aidha, barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilomita 619.29 mwaka 2020 hadi kufikia kilomita 1,302.55 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 110.3.

Vilevile, idadi ya madaraja imepanda kutoka 92 mwaka 2020 hadi 130 mwaka 2025, huku makalvati yakiongezeka kutoka 1,142 hadi 2,071 katika kipindi hicho. Taa za barabarani zimeongezeka kutoka 238 mwaka 2020 hadi 807 mwaka 2025, hatua inayosaidia kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara.

Kwa upande mwingine, madaraja ya mawe yameongezeka kutoka 49 mwaka 2020 hadi 150 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 206. Barabara zenye kiwango cha zege pia zimeongezeka kutoka kilomita 1.02 mwaka 2020 hadi kilomita 6.89 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 575.

Maendeleo hayo yamechochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi mkoani Kigoma, ambapo pato la mkoa limepanda kutoka shilingi trilioni 4.1 mwaka 2020 hadi shilingi trilioni 5.6 mwaka 2024. Pato la mwananchi mmoja nalo limeongezeka kutoka shilingi milioni 1.4 mwaka 2020 hadi shilingi milioni 2.1 mwaka 2024.