MGOMBEA UBUNGE JIMBO JIPYA LA CHAMANZI KUPITIA CHAMA CHA AAFP AAHIDI KUTATUA KERO ZA WANANCHI
Na Neema Mpaka, Dar es Salaam – Mgombea Ubunge wa Jimbo jipya la Chamanzi kwa tiketi ya Chama cha Wakulima (AAFP), Shani Kitumbua, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuwatumikia ili kushughulikia changamoto zinazowakabili, ikiwemo ubovu wa barabara, upungufu wa shule na matukio ya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika Halmashauri ya Temeke, mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Fortunata Shija, Kitumbua alisema Jimbo la Chamanzi limeachwa nyuma kimaendeleo licha ya kuwa na idadi kubwa ya wananchi.
“Chamanzi palisahaulika kimaendeleo. Shule ni chache, wanafunzi ni wengi. Mimi kama Mbunge nitahakikisha tunaboresha mazingira ya elimu na kuondoa utaratibu wa wanafunzi kuombwa fedha kila mara wakisingiziwa ada ya masomo ya ziada siku za mapumziko,” alisema Kitumbua.
Aidha, aliahidi kusimamia uboreshaji wa barabara ya Kilungule, akibainisha kuwa hali mbovu ya barabara hiyo imekuwa kero ya muda mrefu na kusababisha changamoto za usafiri kwa wananchi, huku baadhi ya askari wa usalama barabarani wakituhumiwa kuitumia kama chanzo cha kuwakandamiza madereva wa daladala, bajaji na pikipiki kwa rushwa.
Kitumbua alisema iwapo atachaguliwa, atakuwa mstari wa mbele kuisemea Chamanzi Bungeni ili wananchi wake wapate maendeleo sawa na maeneo mengine nchini.