Breaking News

RAIS SAMIA AAJIRI WATAALAMU ZAIDI YA 34,000 KADA YA AFYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameajiri jumla ya wataalamu 34,720 wa kada mbalimbali za afya kwa ajili ya kusambazwa katika vituo vya kutoa huduma za afya ya msingi nchini.

Kati ya walioajiriwa, madaktari ni 1,851, matabibu 6,546, wauguzi 10,213, na wataalamu wa mionzi, macho, maabara, meno na dawa 1,488. Vilevile, wafamasia walioajiriwa ni 993, maafisa lishe 328, maafisa ustawi wa jamii 224, mafundi sanifu wa vifaa tiba 239, huku kada nyingine zikifikia 12,838.

Aidha, jumla ya watumishi 700 wameajiriwa kwa mikataba ya miaka mitatu, pamoja na watumishi 150 waliopata ajira kwa mkataba maalum kupitia mpango wa UVIKO.

Hatua hii inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta hiyo muhimu.