UFAULU WAPAA MATOKEO YA KUHITIMU ELIMU YA MSINGI, SOMO LA ELIMU YA DINI YA KIISLAMU MWAKA 2025
Dar es salaam - Baraza la Mitihani la Tanzania ya Kiislamu (TISTA) limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi katika somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu uliofanyika Agosti 13, 2025 ambapo kwa mwaka 2025 ufaulu uneongezeka hadi kufikia asimilia 97.40.
Akitangaza matokeo hayo mapema leo 25 Agost 2025 kwa niaba ya katibu TISTA, Al Haji Mruna, SheikhYusuph Mussa Kundecha amesema jumla ya shule 4,375 kutoka mikoa 28 na halmashauri 164 zilisajiliwa kushiriki mtihani huo.
Alisema Watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 161,856 wakiwemo wasichana 86,726 (asilimia 53.58) na wavulana 75,130 (asilimia 46.42). Aidha, walioshiriki mtihani ni 146,807 sawa na asilimia 90.70 ya watahiwa wote waliosajiliwa.
Katika matokeo hayo, ufaulu umegawanywa katika madaraja matano (A–E). Watahiniwa waliopata alama za ufaulu (daraja A–D) ni 143,035, sawa na asilimia 97.40 ya wote waliofanya mtihani. Kati yao, daraja A limepata watahiniwa 4,148, daraja B ni 15,321, daraja C ni 52,290 na daraja D ni 71,276, huku daraja E likipata watahiniwa 3,772.
Ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 94.10, mwaka huu kiwango kimeongezeka kwa asilimia 3.50. Ongezeko hilo limeelezwa kuwa ishara ya jitihada za pamoja kati ya walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wa elimu nchini.
TISTA imeishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Wizara ya TAMISEMI, viongozi wa mikoa na halmashauri, walimu na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mtihani huo. Pia imewapongeza watahiniwa kwa kutulia na kuzingatia taratibu za mtihani.