BALOZI MATINYI AKUTANA NA WANAFUNZI WA TANZANIA NCHINI SWEDEN
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amekutana na wanafunzi wapya wa Kitanzania waliopata nafasi ya kusoma shahada za uzamili katika fani mbalimbali nchini humo kwa mwaka wa masomo 2025/26.
Hafla hiyo fupi ilifanyika Jumapili, Septemba 21, 2025, katika makazi ya Balozi jijini Stockholm, na kuhudhuriwa pia na maafisa watano wa Ubalozi wa Tanzania.
Akizungumza na wanafunzi hao, Balozi Matinyi aliwataka kutumia maarifa na fursa walizopata kwa manufaa ya taifa baada ya kumaliza masomo yao. Alisisitiza kuwa elimu wanayoipata nje ya nchi ni rasilimali muhimu katika kuchochea maendeleo ya Tanzania.




