Breaking News

MSAMA AWASIHI WATANZANIA KUTUNZA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Na Neema Mpaka, Dar es salaam - Aliyewahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, Alex Msama, amewataka Watanzania kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa uchaguzi utapita lakini maisha yataendelea.

Akizungumza leo Oktoba 20, 2025, jijini Dar es Salaam, Msama amesema hakuna sababu ya kuwa na hofu kwani vyombo vya usalama vimewahakikishia wananchi ulinzi wa kutosha kipindi chote cha uchaguzi.

Aidha, Msama amewahimiza wakazi wa jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kampeni za mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ambazo zinatarajiwa kuanza kesho.

“Niwaombe ndugu zangu wa dini zote na Watanzania wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kumpokea mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, Samia Suluhu Hassan, na kushiriki katika kampeni zinazotarajiwa kuanza kesho hapa mkoani Dar es Salaam,” alisema Msama.

Msama amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, akibainisha kuwa amani ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa.