Breaking News

BODI YA WAKURUGENZI WA KAMPUNI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA LONGIDO YAZINDULIWA, DED ATOA MAELEKEZO

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassor Shemzigwa, tarehe 18 Disemba 2025, amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Kibiashara ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido Oldonyo Nothern Company Limited, tukio lililoambatana na kikao cha kwanza cha bodi hiyo kwa ajili ya kuweka mikakati ya uendeshaji wa kampuni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw. Shemzigwa aliwapongeza wajumbe wa bodi kwa kuaminiwa na kupewa jukumu la kuisimamia kampuni hiyo, ambayo miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia kiwanda cha uzalishaji wa matofali cha Halmashauri.

“Siku ya leo ni siku ya furaha kubwa kwangu, ni siku ambayo nimekuwa nikiitamani kwa muda mrefu kuona kampuni hii inaanza rasmi. Tuliamua kuanzisha kampuni hii baada ya kupitia changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa kiwanda cha matofali, hivyo tukiona ni vyema kuanzisha kampuni ya Halmashauri,” alisema Bw. Shemzigwa.
Alisisitiza kuwa bodi hiyo inapaswa kufanya kazi kwa mshikamano na kama timu moja ili kufikia matokeo ya haraka, akieleza kuwa Halmashauri ina rasilimali za kutosha pamoja na wataalamu wenye weledi wa kutekeleza mipango kwa ufanisi.

Bw. Shemzigwa aliongeza kuwa jukumu walilopewa linahitaji kujitoa kwa dhati usiku na mchana ili kuhakikisha kampuni inasonga mbele, huku akiahidi kutoa ushirikiano wa karibu na kuiunga mkono kampuni hiyo katika hatua zake za awali kabla haijisimamia kikamilifu.
Aidha, aliielekeza bodi hiyo kuhakikisha inaweka vipaumbele sahihi katika utekelezaji wa majukumu yake, na kumuagiza Mtendaji Mkuu wa Kampuni kuhakikisha kampuni inatoa gawio na kuchangia ongezeko la mapato ya Halmashauri, hususan katika Mwaka wa Fedha wa 2026/2027.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Rajabu Mmunda, aliishukuru Menejimenti ya Halmashauri kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo. Aliahidi kuwa bodi itafanya kazi kwa ushirikiano na kwa weledi ili kuleta tija kwa kampuni na kupata matokeo chanya kwa wakati mfupi.