Breaking News

TMA KUTOA RASMI UTABIRI WA MVUA ZA MASIKA MWEZI UJAO

Na Mwandishi Wetu - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za Masika mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, utabiri utakaohusu kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei.

Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Alfred Kondoya, amesema utabiri huo una umuhimu mkubwa katika kusaidia mipango ya sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, maji, nishati pamoja na miundombinu.

Kondoya amesema mvua za Masika zina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo utabiri wake huisaidia Serikali, wadau na wananchi kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya hewa unaotarajiwa.

Amesisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa taarifa hiyo, wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu na kusubiri tangazo rasmi la TMA badala ya kutegemea taarifa zisizo rasmi ambazo zinaweza kupotosha.
Aidha, TMA imeeleza kuwa kabla ya kutangaza utabiri wa mvua za Masika, hufanya maandalizi ya kina ikiwemo ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za hali ya hewa kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Kondoya, mamlaka hiyo pia hufanya vikao vya ushauri na taasisi za Serikali pamoja na wadau muhimu ili kuhakikisha utabiri unaotolewa unazingatia mahitaji ya sekta husika.

Baadhi ya taasisi zinazoshirikishwa katika mchakato huo ni pamoja na Wizara ya Maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi nyingine za umma na binafsi.

TMA imesema ushirikishwaji wa wadau hulenga kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua na kutoa ushauri wa kitaalamu unaolenga kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa.

Source Touch Media