RAIS SAMIA KUFUNGUA RASMI SOKO LA KARIAKOO FEBRUARI 8, 2026
Dar es Salaam - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua na kuzindua rasmi Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam tarehe 8 Februari, 2026.
Akizungumza leo Februari 6, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema uzinduzi huo unahusisha soko la zamani lililopata ajali ya moto na kufanyiwa ukarabati mkubwa, pamoja na ujenzi wa soko jipya la kisasa.
Mhe. Chalamila amesema Soko la Kariakoo limekamilika kwa asilimia 100, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 28 zimetumika katika ukarabati na ujenzi wa soko jipya lenye takribani vizimba zaidi ya 1,500 kwa ajili ya wafanyabiashara.
“Mhe. Rais atafanya ufunguzi na uzinduzi wa Soko la Kariakoo lililoungua na kufanyiwa ukarabati, sambamba na soko jipya lililojengwa kwa viwango vya kisasa,” amesema Mhe. Chalamila.
Aidha, amewataka wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao katika soko hilo kabla ya tukio la moto, pamoja na wamachinga wa jijini Dar es Salaam, kujitokeza kwa wingi siku ya uzinduzi ili kushuhudia tukio hilo muhimu la kihistoria.
Vilevile, Mhe. Chalamila amewaagiza wafanyabiashara wadogo waliovamia na kufunga barabara za kuingia katika Soko la Kariakoo kuondoka mara moja na kuziacha barabara hizo wazi kabla ya Februari 8, 2026, ili kuruhusu wafanyabiashara kuingia na kuanza shughuli zao ndani ya soko hilo.
Uzinduzi wa Soko la Kariakoo unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha biashara, kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa wafanyabiashara pamoja na Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla.




