TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA 2026: MAENEO YA PWANI NA KANDA YA ZIWA YATARAJIWA KUPATA MVUA NYINGI, YATOA TAADHARI KWA SEKTA MBALIMBALI
Dar es Salaam - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2026, ikieleza kuwa maeneo mengi ya pwani ya kaskazini na baadhi ya ukanda wa Ziwa Victoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku nyanda za juu kaskazini mashariki zikitabiriwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi amesema, mvua za Masika zinahusisha maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, yakiwemo nyanda za juu kaskazini mashariki (Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Pwani, visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Mwanzo na Mwisho wa Msimu
TMA imeeleza kuwa mvua za Masika zinatarajiwa kuanza: Wiki ya nne ya Februari hadi wiki ya kwanza ya Machi 2026 katika ukanda wa Ziwa Victoria,
Wiki ya kwanza hadi ya pili ya Machi katika maeneo ya pwani ya kaskazini,
Wiki ya pili hadi ya tatu ya Machi katika nyanda za juu kaskazini mashariki.
Mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya Mei na wiki ya kwanza ya Juni 2026, huku ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Aprili.
Mgawanyo wa Mwelekeo wa Mvua
Kwa mujibu wa TMA:
Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini, mikoa ya Kagera, Geita na kaskazini mwa Kigoma.
Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika nyanda za juu kaskazini mashariki na baadhi ya mikoa ya Ziwa Victoria ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu.
Hata hivyo, TMA imeonya kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa za muda mfupi, yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotabiriwa kupata mvua za chini ya wastani.
Athari Zinazotarajiwa
Mvua nyingi zinaweza kusababisha:
Mfuriko na unyevu kupita kiasi shambani,
Uharibifu wa miundombinu,
Kuenea kwa magonjwa ya mimea, mifugo na binadamu,
Changamoto katika sekta ya usafiri, ujenzi na maji.
Kwa upande mwingine, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache yanaweza kukumbwa na upungufu wa maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo na mifugo.
Ushauri kwa Sekta Mbalimbali
TMA imetoa ushauri mahsusi kwa sekta mbalimbali ikiwemo:
Kilimo: Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kutumia mbinu za kuhifadhi maji, kudhibiti magonjwa na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani.
Mifugo na Uvuvi: Wafugaji wahimizwa kupanga matumizi ya maji na malisho, na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mifugo.
Usafiri na Ujenzi:
Wadau wanashauriwa kufuatilia utabiri wa kila siku ili kupunguza athari za mafuriko na kuchelewa kwa miradi.
Afya: Jamii zimetakiwa kutumia maji safi na salama na kuchukua hatua za kudhibiti magonjwa ya mlipuko yanayohusiana na maji na wadudu.
Serikali za Mitaa: Zimehimizwa kuimarisha mifumo ya maji, mifereji ya maji ya mvua na mipango ya kudhibiti maafa.
Wito kwa Umma
TMA imesisitiza kuwa mwelekeo huu ni wa jumla kwa msimu mzima, hivyo wananchi na wadau wanahimizwa kuendelea kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi pamoja na tahadhari rasmi zitakazotolewa mara kwa mara.
“Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ni msingi muhimu wa kulinda maisha, mali na kukuza uchumi,” imeeleza TMA.





