Breaking News

ASKOFU LYIMO AWATAKA WAZAZI KUIMARISHA MALEZI YA KIIMANI KWA WATOTO

Bariadi – Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo jipya la Bariadi, Mhashamu Prosper Lyimo, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto ili wakue wakimjua Mungu na kuishi kwa maadili bora ya Kikristo.

Askofu Lyimo ametoa wito huo wakati wa homilia aliyoitoa leo katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Kigango cha Mtakatifu Mathayo Kidinda, ambapo alisisitiza umuhimu wa familia kudumisha wito wa ndoa ili kukuza miito ya utumishi katika Kanisa.

Amesema Kanisa Katoliki linaendelea kuwa sehemu muhimu ya malezi ya jamii, likilea watoto kiroho, kielimu na kiafya ili kujenga taifa lenye misingi imara ya maadili.

“Malezi ya watoto ni muhimu sana, majitoleo na kuleta familia katika wito wa ndoa ili kupata watumishi wengi shambani mwa Bwana kupitia miito mitakatifu ya Upadre na Usista. Watoto wakitaka kumtumikia Mungu muwaruhusu,” amesema Askofu Lyimo.

Aidha, amewahimiza waumini kuimarisha malezi ya kiimani ndani ya familia na kuwahamasisha watoto kujiunga na vyama vya kitume kama njia ya kukuza imani na maadili.

“Familia tuzingatie malezi na miito, tusisitize katika familia zetu. Mjiunge na vyama vya kitume, muwaruhusu watoto kujiunga na vyama hivyo,” ameongeza.

Katika hotuba yake, Askofu Lyimo pia ameeleza kuwa Jimbo la Bariadi linaendelea kuweka mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu, akiwataka viongozi na waumini kushirikiana katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Vilevile, amewasisitiza waumini kuendeleza maeneo ya vigango na parokia kwa kupanda miti ili kulinda maeneo hayo dhidi ya uharibifu, ikiwemo uvamizi wa mifugo, sambamba na kuweka mipango ya kupanua maeneo kwa ajili ya huduma za Kanisa kwa siku zijazo.

“Tunatoa huduma kiroho na kimwili, tupange kuangalia kuongeza maeneo huko mbele miaka 20 ili tuendeleze kigango chetu, tunatembea kwa pamoja hatua kwa hatua,” amesema.