DC MAGOTI AWAASA VIJANA KUWA WAZALENDO NA KUTIMIZA WAJIBU KATIKA JAMII ZAO
Kisarawe - Wilaya ya Kisarawe imeendesha kongamano la vijana (Vijana Platform) katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, likiwa na lengo la kutoa elimu juu ya uraia, pamoja na kuhamasisha umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano miongoni mwa vijana.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Tito Magoti, alisema kuwa uongozi wa wilaya umeanzisha utaratibu wa “kijiwe mtaa kwa mtaa” unaolenga kuwafikia vijana katika kata mbalimbali ili kujadiliana nao masuala ya maendeleo, hususan wajibu wao katika kulinda amani na kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Alieleza kuwa mbinu hiyo imewasaidia viongozi kuwa karibu zaidi na vijana, akibainisha kuwa wamekuwa wakikutana nao katika mazingira ya kawaida ili kujenga ukaribu na kuwasikiliza kwa karibu.
“Tumekuwa karibu na vijana, tumekutana nao na kujadiliana mambo mbalimbali ili kuwajengea uelewa wa umuhimu wa kulinda na kutunza amani tuliyonayo,” alisema Magoti.
Aidha, alibainisha kuwa wilaya inaendelea kuimarisha sera ya kuwawezesha vijana kupitia elimu ya ujasiriamali, uzalendo pamoja na upatikanaji wa mikopo. Aliongeza kuwa serikali ya wilaya imetenga maeneo ya kilimo, ambapo vijana wanaweza kupatiwa hadi hekari mbili kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya aliwahimiza vijana kuzingatia maadili mema, kutimiza wajibu wao katika jamii na kuepuka vitendo visivyofaa kama matumizi ya pombe kupita kiasi na uvutaji sigara.
Pia aligusia changamoto ya vijana kuogopa kufika katika ofisi za umma kueleza matatizo yao, akisisitiza kuwa serikali imeweka mifumo na taasisi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo bila hofu.
Magoti aliwahimiza vijana kutumia vyema mikopo wanayopata kwa kuwekeza katika shughuli za maendeleo ili waweze kurejesha kwa wakati, hatua itakayowezesha wengine kunufaika na mikopo hiyo baadaye.
Vilevile, aliwataka vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya wilaya, ikiwemo kushiriki katika mbio za Mwenge wa Uhuru na kutembelea miradi ya maendeleo itakayopitiwa na mwenge huo.
Akihitimisha, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa rai kwa vijana kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana, ikiwemo mikopo na mashindano ya kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na uzalendo. Alisisitiza kuwa pindi wanapoona au kukutana na changamoto yoyote, wanapaswa kufikisha taarifa kwa mamlaka husika bila kusita.




