DOYO AWAHIMIZA VIJANA KUWA MABALOZI WA AMANI, AIUNGA MKONO TUME YA JAJI CHANDE
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema ana matumaini makubwa na Tume ya Jaji Chande inayochunguza matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa tume hiyo, Doyo alisema imani yake inatokana na muundo wa wajumbe wake, akieleza kuwa imeundwa na watu wenye uzoefu mkubwa wakiwemo majaji wastaafu, mawaziri wa zamani pamoja na viongozi waandamizi waliowahi kushika nafasi mbalimbali katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema kutokana na weledi huo, Watanzania wanapaswa kutarajia ripoti yenye kuzingatia haki na kukidhi matarajio ya umma.
Wakati huo huo, Doyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha utulivu na kuipa nafasi tume hiyo kukamilisha majukumu yake bila shinikizo lisilo la lazima.
“Ni muhimu Watanzania wakaendelea kuwa watulivu na kuiamini tume inapotekeleza majukumu yake, badala ya kuanza kutoa mashinikizo ambayo yanaweza kusababisha kuvunjika kwa amani, umoja na mshikamano tulionao,” alisema.
Aidha, aliwataka vijana kuchukua nafasi ya kuwa mabalozi wa amani kwa kuhamasisha mshikamano wa kitaifa kupitia majukwaa mbalimbali, hususan mitandao ya kijamii, badala ya kuchochea migawanyiko.
Pia alisisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa zilizopo kiuchumi ili kujikwamua kimaisha, akieleza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea mchango wao katika kujenga jamii yenye mshikamano na ustawi.




