KAULI ZA WANASIASA ZATAJWA KUCHOCHEA MACHAFUKO: SOMO KUTOKA TUME YA JAJI CHANDE
Na Mwandishi Wetu - Watanzania wametakiwa kupuuza Kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa ambazo kutajwa kama moja ya vyanzo vikuu vya migogoro ya kijamii na kisiasa nchini, hasa pale zinapokosa uwajibikaji na tahadhari.
Kauli hiyo imesisitizwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mwanga, Lembrus Mchome, alipokuwa akizungumzia matukio ya machafuko yaliyotokea Oktoba 29.
Kwa mujibu wa Mchome, matamshi ya kisiasa yasiyopimwa yamechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea taharuki miongoni mwa wananchi na hatimaye kusababisha vurugu. Anasisitiza kuwa kauli hizo zimekuwa na athari kubwa zaidi kuliko inavyodhaniwa, na kwamba viongozi wanapaswa kuwa makini na maneno wanayoyatoa hadharani.
Akirejea ripoti ya Tume ya Jaji Chande iliyochunguza matukio hayo, Mchome anaeleza kuwa licha ya kuwepo kwa mapungufu machache, tume hiyo ilikuwa miongoni mwa tume bora kuwahi kuundwa. Anaipongeza kwa kutoa uchambuzi mpana na mapendekezo yenye lengo la kuimarisha hali ya utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Mchome anabainisha kuwa moja ya mambo muhimu yaliyojitokeza katika ripoti hiyo ni namna kauli za wanasiasa zilivyochangia kuibua hisia kali kwa wananchi. Kwa mtazamo wake, hili linapaswa kuwa fundisho kwa viongozi wote wa kisiasa kuwa na nidhamu ya lugha wanapowasiliana na umma.
Aidha, ameitaka serikali kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na tume hiyo bila kusuasua, akiamini kuwa utekelezaji wake utasaidia kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo siku zijazo.
Kwa ujumla, hoja ya Mchome inaibua mjadala mpana kuhusu wajibu wa viongozi katika kulinda amani kupitia kauli zao.
"Maneno yana nguvu kubwa yanaweza kujenga au kubomoa. Hivyo basi, uwajibikaji katika matamshi ya kisiasa si hiari bali ni wajibu wa msingi kwa mustakabali wa taifa". Alisema Mchome




