Breaking News

MAJADILIANO NDIYO NJIA BORA YA KUTATUA MIGOGORO – GERTRUDE MONGELA

Mwanasiasa na mwanadiplomasia wa kimataifa, Gertrude Mongela, amesisitiza umuhimu wa majadiliano kama njia bora ya kukabiliana na migogoro na changamoto zinazoikumba dunia ya sasa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mongela aliyewahi kuwa Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake alisema dunia inakabiliwa na hali ya lawama kati ya vizazi, hususan wazee na vijana, jambo linalohitaji busara na mazungumzo ya wazi ili kupata suluhu ya kudumu.

Alieleza kuwa mabadiliko makubwa ya tabianchi, uchumi, siasa na teknolojia yameathiri kwa kiasi kikubwa mienendo ya jamii, na hivyo kuna ulazima wa kujitathmini upya ili kuendana na hali halisi bila kuleta migongano isiyo ya lazima.

Akizungumzia mabadiliko ya malezi, Mongela alibainisha kuwa uhusiano wa karibu kati ya wazazi na watoto umedorora ikilinganishwa na zamani. Alikumbusha kuwa hapo awali watoto walilelewa kwa ukaribu mkubwa na wazazi wao, tofauti na sasa ambapo wengi hukulia chini ya malezi ya watu wengine.

Aidha, aligusia kupungua kwa mamlaka ya baba ndani ya familia, akieleza kuwa hapo awali baba alikuwa na nafasi thabiti ya uongozi iliyosaidia kuweka nidhamu na mwelekeo kwa watoto. Hata hivyo, aliongeza kuwa hali ya sasa imekuwa changamoto kwa vijana, ambao wanahitaji zaidi ya matumaini ili kukabiliana na ugumu wa maisha, ikiwemo changamoto za mahusiano na ndoa.

Kuhusu mvutano wa kizazi, Mongela alionya dhidi ya tabia ya wazee kuwalaumu vijana pekee kwa matatizo ya kijamii. Alisema kufanya hivyo ni kuwaonea, kwani hata baadhi ya wazee wamechangia changamoto zilizopo.

Alisisitiza umuhimu wa kutumia busara na majadiliano badala ya lawama, akitoa mfano wa kisa alichokutana nacho wakati akiwa mbunge huko Ukerewe, ambapo mzee mmoja alikiri kuwa kama angekumbana na changamoto za sasa katika ujana wake, huenda naye angeathirika.

“Hii inatufundisha kuwa badala ya kunyoosheana vidole, tunapaswa kukaa pamoja na kutumia majadiliano kupata suluhisho la pamoja,” alisema.

Akizungumzia harakati za kudai uhuru na usawa, Mongela alitoa mifano ya wanawake waliotumia hoja na ujasiri kuleta mabadiliko bila kutumia vurugu, akiwemo Binti Matola. Alieleza kuwa ujasiri wa kweli unatokana na uwezo wa kufikiri kwa kina na kuwasilisha hoja zenye kujenga.

Kwa kuhitimisha, Mongela alitoa wito kwa jamii kutumia majukwaa mbalimbali kama makanisa, misikiti na vyombo vya uwakilishi kujadili masuala ya kitaifa kwa lengo la kujenga mustakabali bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.