Breaking News

RAIS SAMIA AONGOZA UGAWAJI WA MITUNGI YA GESI, ASISITIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KWA MAMA NA BABA LISHE

Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan ameongoza zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi kwa mama na baba lishe ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Tukio hilo limefanyika Aprili 21, 2026 katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre jijini Dar es Salaam, likiwa sehemu ya Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe lililowakutanisha wajasiriamali wa sekta ya chakula kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika kulinda afya za wananchi na mazingira. Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa wananchi wote.
Aidha, alibainisha kuwa matumizi ya gesi ya kupikia yatasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hali ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya, hususan kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za upishi.

Kwa upande wao, baadhi ya mama na baba lishe walionufaika na mpango huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema itarahisisha shughuli zao za kila siku, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi katika huduma wanazotoa kwa wateja wao.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kukuza matumizi ya nishati safi nchini, sambamba na kuwawezesha wajasiriamali wadogo ambao wana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.