ACT WAZALENDO YACHAMBUA RIPOTI YA TUME YA JAJI CHANDE
Chama cha ACT Wazalendo kimeendelea kusisitiza msimamo wake wa kutoiamini wala kuitambua Tume ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan chini ya uenyekiti wa Mohamed Chande Othman.
Chama hicho kimeeleza kuwa ripoti iliyowasilishwa na tume hiyo imeshindwa kutoa ukweli kamili kuhusu matukio ya mauaji yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo, huku kikidai kuwa ripoti hiyo imelenga kuwalinda baadhi ya watu waliohusika na vitendo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya ACT-Wazalendo yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita, amesema kuwa ripoti ya tume hiyo imejaa mapungufu makubwa, ikiwemo kutokuwepo kwa takwimu sahihi za watu waliopoteza maisha katika vurugu hizo.
Kwa mujibu wa Mchinjita, ripoti hiyo pia haijaweka bayana hatua mahsusi zitakazochukuliwa dhidi ya wahusika wa mauaji na wale waliotuhumiwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kulinda usalama wa wananchi wakati wa vurugu hizo.
ACT-Wazalendo imeendelea kudai kuundwa kwa tume huru ya kimataifa chini ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufanya uchunguzi mpya wa kina kuhusu matukio hayo, ikieleza kuwa Tanzania ni mwanachama wa jumuiya hiyo na hivyo ina wajibu wa kuruhusu uchunguzi huru na wa haki ili ukweli ujulikane.
Aidha, chama hicho kimedai kuwa viongozi mbalimbali wa serikali na vyombo vya ulinzi wanapaswa kuwajibishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni uzembe wa kushindwa kuzuia mauaji na vurugu hizo licha ya kuwepo kwa taarifa za mipango ya uvunjifu wa amani karibu na maeneo ya vituo vya polisi.
Mchinjita amesema viongozi wanaopaswa kuchukuliwa hatua ni pamoja na wakuu wa mikoa ambako vurugu hizo zilitokea pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama waliokuwa na jukumu la kusimamia hali ya amani katika maeneo hayo.
Kauli hiyo inaendelea kuongeza mjadala wa kisiasa kuhusu ripoti ya Tume ya Jaji Chande, huku wadau mbalimbali wakitoa maoni tofauti kuhusu uwajibikaji, maridhiano ya kitaifa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo kutokea tena nchini.




