Breaking News

WAZIRI MAKONDA: VYOMBO VYA HABARI JIJENGEENI UWEZO WA KIUCHUMI, ACHENI “KUWABRAND” WANASIASA

Na mwandishi wetu - Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amevitaka vyombo vya habari nchini kuacha tabia ya kuwajenga watu binafsi kwa maslahi yao, wakiwemo wanasiasa wasio na mwelekeo, na badala yake kujikita katika mbinu bunifu za kitasnia zitakazoviwezesha kujiimarisha kiuchumi.

Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kuandaa na kusukuma ajenda zenye manufaa kwa taifa, hatua itakayochangia si tu maendeleo ya sekta ya habari bali pia ustawi wa jamii kwa ujumla.

Akizungumza jijini Arusha wakati akifunga kongamano la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Makonda amesema kuwa uhuru wa kweli wa habari hauwezi kufikiwa ikiwa wanahabari wataendelea kukabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Ameeleza kuwa uhuru wa habari unapaswa kuendana na uwezo wa kiuchumi wa wanahabari, akionya kuwa hali ya umasikini huwafanya baadhi yao kuathiriwa na ushawishi wa watu wenye maslahi binafsi, jambo linalodhoofisha misingi ya taaluma hiyo.

Aidha, amesema wizara ipo tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya habari pamoja na mashirika mbalimbali ili kuhakikisha maazimio yaliyopitishwa katika kongamano hilo yanatekelezwa kikamilifu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Media Council (TMC), Asha Abinallah, amesema wadau wa habari wamekubaliana mambo 11 muhimu ambayo yamewasilishwa kwa serikali kwa ajili ya utekelezaji.