Breaking News

WIZARA ZA VIJANA BARA NA VISIWANI KUSHIRIKIANA KUENDESHA PROGRAMU ZA VIJANA

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Dkt. Kedmon Mapana amesema kwamba Wizara ya Maendeleo ya Vijana itaendelea kushirikiana na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji ya Zanzibar katika kuratibu majukwaa ya vijana na programu za kuwezesha vijana kiuchumi nchini.

Amesema hayo leo Aprili 21, 2026 alipofanya kikao na Baraza la Vijana kutoka Wilaya ya Mjini, Zanzibar, lililofanya ziara ya mafunzo katika Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana iliyopo Mji wa Serikali.
Katika kikao hicho Dkt. Mapana ameeleza kuhusu majukumu, shughuli na mipango ya Wizara katika kuwawezesha vijana, ikiwa ni pamoja na kuratibu na kuendesha majukwaa ya vijana pamoja na kutekeleza programu za uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia mikopo.

Dkt. Mapana amesema kuwa mipango ya Wizara ni pamoja na kuanzisha mfumo utakaowezesha kupata taarifa za vijana, zitakazorahisha na kuleta ufanisi katika kuratibu masuala ya vijana kama kazi na fursa mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Rajabu Makame Ali ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema kwamba Vijana wa Wilaya ya Mjini wako tayari kushiriki kikamilifu katika programu zote za vijana zitakazoratibiwa na wizara, ikiwemo majukwaa ya vijana na mashindano ya mawazo ya kiuchumi yanayolenga kuleta suluhu ya changamoto zinazolikabili taifa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Maya Hamad Ali amebainisha kuwa ziara ya Baraza hilo imekuwa na mafanikio kwani imewawezesha kujifunza kuhusu uongozi wa vijana, uratibu wa programu za vijana, pamoja na namna ya kutafuta na kutengeneza fursa kwa ajili ya vijana.