Breaking News

MCHOME: VIJANA JIKITENI KWENYE KAZI, EPUKENI SIASA ZISIZO NA TIJA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mwanga, Lembrus Mchome, ametoa wito kwa vijana kujikita katika shughuli za maendeleo badala ya kupoteza muda kwenye harakati za kisiasa zinazoweza kuchochea vurugu na kuharibu mustakabali wao.

Akizungumza katika mahojiano maalum kuhusu nafasi ya vijana katika kulinda amani na utulivu wa nchi, Mchome amesema baadhi ya vijana wamekuwa wakipoteza mwelekeo kutokana na kushawishiwa kujiingiza katika vitendo visivyo na tija, ambavyo wakati mwingine huacha madhara makubwa ikiwemo ulemavu au kupoteza fursa za maendeleo.

Amesisitiza kuwa ujana ni kipindi cha nguvu na ubunifu, hivyo ni muhimu nguvu hizo zielekezwe katika shughuli za kiuchumi kama biashara, ajira na ujasiriamali ili kujenga maisha bora.

“Ni vyema vijana wakajiepusha na wanasiasa wanaochochea vurugu zinazoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa taifa. Amani ikitoweka, hata fursa za kujipatia kipato hupotea,” amesema Mchome.

Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuachana na siasa zisizo na tija na badala yake wajikite katika kupambana na changamoto za maisha kwa kufanya kazi halali zitakazowawezesha kufikia malengo yao.

Aidha, amewahimiza vijana kutokata tamaa licha ya changamoto za kimaisha, bali wawe wabunifu na wachangamkie fursa mbalimbali zilizopo ili kujiletea maendeleo binafsi na ya familia zao.

Mchome alihitimisha kwa kusisitiza kuwa amani ya nchi inategemea utulivu wa vijana, na utulivu huo hujengwa pale vijana wanapokuwa na shughuli halali zinazowaingizia kipato.