Breaking News

TAHLISO YAWATAKA VIJANA KUWA MSTARI WA MBELE KULINDA AMANI NA KUKEMEA UPOTOSHAJI

Dar es salaam - Rais wa Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu nchini (TAHLISO), Geofrey Kiliba, ametoa mwito kwa vijana kote nchini kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa taifa hili.

Akizungumza na wanahabari Mei 2, 2026, Kiliba amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia maarifa na karama zao mbalimbali kuhubiri utulivu na kuzuia viashiria vyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi, akibainisha kuwa itakuwa ni ukosefu wa hekima kwa kundi hilo kukaa kimya wakati kukiwa na mienendo inayolenga kulibomoa taifa. 

Amewataka vijana kutokubali kuyumbishwa na hofu, vitisho, wala ulaghai wa aina yoyote, badala yake wasimame imara kukemea upotoshaji na misingi ya uanaharakati isiyo na tija ambayo haileti heshima wala kuvumiliana miongoni mwa Watanzania.

Katika maelezo yake yaliyojaa uzalendo, Kiliba ameweka wazi kuwa taifa linapoharibika kutokana na kupuuza au uoga wa kusema ukweli, kundi litakaloumia zaidi ni vijana wenyewe, hivyo wanapaswa kuwa kikosi cha kwanza kulinda tunu za taifa ambazo zimekuwa zikienziwa kwa muda mrefu.

Amesema, "Itakuwa sio hekima, wala sio sawa hata kidogo tukakaa kimya juu ya haya mambo yote yanayoendelea, hasa yale yanayofanywa na baadhi ya watu wachache yanayolenga kulibomoa taifa hili; tuna kila sababu ya kuhakikisha kwa maarifa tuliyonayo tunabeba ajenda ya kuhubiri amani, umoja na mshikamano." 

Kiongozi huyo amewahimiza vijana kutokukubali kukosa nguvu ya kuchukua hatua za kizalendo za kulipigania taifa ili liendelee kubaki salama, akisisitiza kuwa ni lazima kila anayebeba ajenda zisizoleta tija aambiwe ukweli kwa uwazi kuwa mambo hayo hayakubaliki.

Kauli hiyo ya Kiliba imepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi katika majukwaa ya kijamii, ambapo wengi wameonekana kuunga mkono msimamo wake wakimtaja kama kiongozi mwenye uchungu na nchi yake. 

Baadhi ya maoni ya mtandaoni yamekwenda mbali zaidi kwa kuitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaodaiwa kueneza propaganda na chuki ambazo zinaweza kuchochea machafuko na kuivuruga amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Wananchi hao wameeleza kuwa kuna haja ya kuweka mipaka iliyo wazi kati ya kutoa maoni na majaribio ya kuishinikiza serikali kwa namna inayovuka misingi ya kisheria, huku wakisisitiza kuwa kuendelea kuwachekea watu wanaopandikiza fujo kunaweza kulifikisha taifa kwenye hatua mbaya ya kupoteza utulivu uliopo.