FAHARI YA TANZANIA HAIKO KWENYE PICHA... NJOO UIONE KWA MACHO YAKO
Na Beatus Maganja - "Asiyefika kwao, huamini kwao hakuna." Hivyo ndivyo walivyotuasa wahenga. Lakini leo kuna ukweli mwingine unaotugusa. Wapo Watanzania wanaowajua simba kupitia televisheni kuliko walivyowahi kuwaona wakiwa hai. Wapo wanaowafahamu fisi kupitia hadithi za utotoni kuliko walivyowahi kuwaona mubashara. Wapo wanaosafiri maelfu ya kilomita kutafuta maajabu ya dunia, ilhali maajabu hayo yapo ndani ya nchi yao.
Hebu jiulize... ulijisikiaje mara ya kwanza ulipomwona simba? Si kwenye simu. Si kwenye YouTube. Bali akiwa hai, akitembea kwa madaha kama mfalme wa nyika. Bila shaka moyo ulidunda tofauti, si ndiyo? Mwili ulisisimka au sio? Ghafla ukagundua kwa nini watu kutoka kila kona ya dunia huja Tanzania kumtazama.
Na fisi je? Kiumbe ambaye wengi humhukumu kwa simulizi walizosikia. Lakini ukisimama mbele yake ndipo unatambua kuwa ni mmoja wa wanyama wenye akili kubwa, mwenye mfumo wa kijamii unaovutia na mchango muhimu katika kusafisha mazingira. Kweli wahenga walisema, "Usiposafiri, hutajua mengi."
Tanzania si tajiri kwa dhahabu pekee. Utajiri wetu mkubwa unatembea, unapiga kelele, unaruka na unaishi kwenye misitu, hifadhi na mapori yetu. Huu ni urithi ambao mataifa mengi hutamani kuwa nao, lakini sisi tumepewa bure na Mwenyezi Mungu. Je, tutauacha ubaki kwenye vitabu au tutaujionea kwa macho yetu?
Ndiyo maana tunasema, Njoo uone. Njoo ujionee fahari ya nchi yako. Njoo ukutane ana kwa ana na wanyamapori ambao wameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi maarufu duniani kwa utalii. Hata kama hujawahi kufika hifadhini, leo unaweza kuanza safari yako kwa kujifunza, kuona na kuuliza.
Na kwa kutambua umuhimu wa kuwafikisha Watanzania karibu zaidi na hazina hii ya kipekee, Wizara ya Maliasili na Utalii imekuja na kauli mbiu ya msimu huu isemayo, "Talii na SabaSaba", mwaliko mahsusi kwa kila Mtanzania na mgeni kujionea vivutio vya utalii, kujifunza na kujivunia urithi wa Taifa letu.
Kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, 2026, karibu utembelee Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 50 ya Kimata





