MAKONDA AWATAKA WANANCHI WA ARUSHA KULINDA AMANI NA KUUNGA MKONO MIRADI YA MAENDELEO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka wananchi wa Arusha kufanya kazi kwa bidii, kuendelea kushirikiana na kulinda amani ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Makonda ametoa wito huo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya AFCON yenye urefu wa kilomita 13 kutoka Moshono hadi Barabara ya Mzunguko ya Morombo.
Amesema Arusha inaendelea kunufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwemo ujenzi wa barabara, hospitali, masoko, stendi za kisasa, viwanja vya michezo, madarasa na kumbi za mikutano.
Aidha, amesema Halmashauri ya Jiji la Arusha inaendelea kufunga taa za kisasa za barabarani kwa lengo la kuboresha mwonekano wa jiji na kuimarisha usalama wa wananchi.
Makonda amemshukuru Rais Samia pamoja na viongozi wengine wa Serikali kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa inalenga kuboresha huduma za kijamii, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuifanya Arusha kuwa jiji la kisasa lenye miundombinu bora.




