NECTA YAWAALIKA WANANCHI SABASABA, YATOA HUDUMA ZA HARQKA ZA VYETI NA ULINGANIFU
Dar es salaam - Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limewahimiza wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kunufaika na huduma mbalimbali za elimu zinazotolewa kwa haraka, ikiwemo utoaji wa vyeti mbadala na ulinganifu wa vyeti.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Uhusiano wa NECTA, John Nchimbi, alisema baraza hilo linashiriki maonesho kuanzia Juni 28 hadi Julai 13 kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza muda wa upatikanaji wake.
Alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na maombi ya vyeti mbadala kwa waliopoteza vyeti vyao na ulinganifu wa vyeti kwa watu waliosoma nje ya Tanzania au katika mifumo ya elimu isiyotumia mtaala wa Tanzania.
Nchimbi alisema kwa utaratibu wa kawaida, mwombaji wa cheti mbadala husubiri hadi siku 30 kukamilisha mchakato, lakini katika kipindi cha maonesho huduma hiyo itatolewa ndani ya siku moja hadi mbili kwa waombaji watakaowasilisha nyaraka zote zinazohitajika.
Alifafanua kuwa mwombaji wa cheti mbadala anatakiwa kuwasilisha tangazo la gazeti la kupoteza cheti, taarifa ya polisi (Loss Report), picha ya pasipoti na nakala ya kitambulisho.
Kwa upande wa huduma ya ulinganifu wa vyeti, alisema waombaji wanapaswa kuwasilisha cheti walichopata kutoka nchi au bodi husika ya mitihani, kitambulisho pamoja na picha ya pasipoti ili huduma hiyo itolewe kwa haraka.
Aidha, aliwahimiza wananchi ambao wamekuwa wakisubiri huduma hizo kwa muda mrefu kutumia fursa ya maonesho hayo, yaliyolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za NECTA.
Alisema banda la NECTA linapatikana katika Banda la Jakaya Kikwete ndani ya viwanja vya Sabasaba, ambapo wataalamu wa baraza hilo wanatoa ushauri, kupokea maombi na kutoa huduma mbalimbali.
Nchimbi pia alitangaza kuwa usajili wa watahiniwa wa kujitegemea wa Mtihani wa Kidato cha Sita umeanza rasmi Julai 1, akiwataka waombaji kufuata taratibu zilizowekwa na kutembelea banda la NECTA kwa maelekezo na msaada wa usajili.
Aliongeza kuwa maafisa wa NECTA wamejipanga kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika banda hilo anapata huduma kwa wakati na bila usumbufu, huku akitoa wito kwa wananchi kutumia kikamilifu kipindi cha maonesho hayo kupata huduma kwa urahisi na kwa muda mfupi kuliko ilivyo katika utaratibu wa kawaida




