Breaking News

NANAUKA: VIJANA WAMEVUNJA DHANA KWAMBA HAWAPENDI KILIMO

Dar es salaam - Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema washiriki wa shindano la Vijana Uchumi Challenge wamewasilisha mawazo ya ubunifu yaliyolenga sekta tisa za kiuchumi zilizoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama sekta za mageuzi.

Nanauka amesema ingawa mawazo yalipokelewa kutoka sekta mbalimbali, sekta ya kilimo imeongoza kwa idadi kubwa ya bunifu zilizowasilishwa, huku zaidi ya asilimia 70 ya mawazo yakihusu kilimo na minyororo ya uongezaji thamani wa mazao ya kilimo.

Amesema jambo hilo limevunja dhana iliyozoeleka kuwa vijana hawapendi kujihusisha na kilimo, kwani wengi wao wameonesha ubunifu unaolenga kuongeza thamani ya mazao badala ya kujikita kwenye uzalishaji wa kawaida pekee.

Aidha, amesema mawazo mengine yaliyowasilishwa yanahusu uanzishwaji wa viwanda, hususan vya kuchakata mazao ya kilimo, pamoja na sekta za ubunifu (creative industries), madini na utalii, ambazo zote ni sehemu ya sekta za kimkakati zinazochochea ukuaji wa uchumi.

Nanauka amesema mawazo hayo yamegusa maeneo mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na yanadhihirisha uwezo mkubwa wa vijana katika kuibua suluhisho zenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Ameongeza kuwa baadhi ya mawazo hayo yatawasilishwa rasmi mbele ya umma wakati wa hatua ya mwisho ya shindano, ambapo washindi watatangazwa.