NCHIMBI AITAKA NEMC KUONGEZA WELEDI, UADILIFU NA KASI YA UHIFADHI WA MAZINGIRA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, amewataka watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kufanya kazi kwa bidii, weledi, ushirikiano na uadilifu huku wakiepuka vitendo vya rushwa ili kuimarisha usimamizi wa mazingira na kuchochea maendeleo ya taifa.
Nchimbi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara katika makao makuu ya NEMC yaliyopo Mikocheni, Dar es Salaam, ambapo aliwataka watumishi kutanguliza maslahi ya taifa na kutokuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia ameipongeza NEMC kwa kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, akisema taasisi hiyo imeendelea kuwa mhimili muhimu katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Makamu wa Rais alisifu Mpango Mkakati wa NEMC wa miaka mitano, akieleza kuwa utaimarisha usimamizi wa mazingira na kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo. Aidha, alisema mashindano ya uhifadhi wa mazingira ni njia muhimu ya kuhamasisha upandaji miti na usafi wa mazingira nchini.
Alisisitiza kuwa, pamoja na kutambua wanaofanya vizuri katika mashindano ya usafi, ni muhimu pia kuwataja hadharani wanaofanya vibaya ili kuongeza uwajibikaji. Hivyo aliiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kushirikiana na NEMC kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.
Nchimbi pia aliitaka NEMC kuongeza msukumo katika matumizi ya nishati safi, teknolojia za kisasa za kuhifadhi mazingira pamoja na kuimarisha usimamizi wa urejelezaji wa taka.
Vilevile, aliwapongeza viongozi wa NEMC kwa hatua wanazoendelea kuchukua za kuibadilisha taasisi hiyo kuwa mamlaka kamili, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imelipa suala hilo kipaumbele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Emmaculate Sware, alisema taasisi hiyo imeandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano (2026/2027–2030/2031) unaolenga kuongeza ufanisi wa usimamizi wa mazingira, kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali, kuboresha ukaguzi na utekelezaji wa sheria, pamoja na kukuza uchumi wa kijani na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Richard Muyungi.








