Breaking News

RAIS DKT. SAMIA TUMEYACHUKUA MAANGALIZO TUTAYAFANYIA KAZI

Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu amesema amechukua angalizo lilitolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Jacob John Mkunda la kufanya mchakato wa kuchambua Wakimbizi na kuona jinsi ya kuwarudisha kwao ambapo amesema anakwenda kulifanyia kazi.

Akiongea leo January 22,2024 wakati wa Mkutano wa Saba wa CDF na Makamanda Jijini Dar es salaam, Rais Samia amenukuliwa akisema “Mimi kama Mkuu wa Nchi nimechukua lile angalizo ulilotupa CDF, la kufanya mchakato wa kuchambua Wakimbizi hasa kutoka Burundi na DRC na kwingineko na kuona jinsi ya kuwarudisha, tumefanya kazi hii kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na lile Shirika linaloshughulika na Wakimbizi Duniani lakini ukweli ni kwamba lile Shirika sasa limeishiwa nguvu kwahiyo ule moto wa kurudisha Wakimbizi kama walivyokuwa wakifanya umepungua”

“Kwahiyo tutaendelea na mazungumzo ya kisiasa baina yetu na Nchi jirani ili tuone njia bora za kurudisha Wakimbizi wale na kama ulivyosema wengine sio Wakimbizi wanaishi kama Raia na wanajiona kama Watanzania, kwahiyo hili kama angalizo tumelichukua na tunakwenda kulifanyia kazi, wito wangu ni kujiimarisha kiteknolojia”

Mapema leo CDF Mkunda aliiomba Serikali ifanye uhakiki ili kuwaondoa Nchini Wakimbizi waliofutiwa hadhi, Wahamiaji haramu na Waomba hifadhi wasiokuwa na sifa za kupewa hadhi ya ukimbizi kutokanana Watu hao kuwa tishio la kiusalama kwani taarifa zilizopo ni kwamba wapo Wakimbizi na Waomba hifadhi ambao wameajiriwa Serikalini na wengine wamepewa teuzi Serikalini katika nafasi zenye maamuzi.