DKT. MPANGO: UWEKEZAJI KATIKA MIUNDOMBINU UNATOKANA NA UBORESHAJI WA MAPATO NA MASOKO YA MITAJI
Abidjan, Ivory Coast – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesema maendeleo makubwa ya Tanzania katika ujenzi na uendelezaji wa miundombinu yanatokana na mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, ushiriki wa sekta binafsi na uimarishaji wa masoko ya mitaji na dhamana.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati wa majadiliano ya viongozi wa juu kuhusu “Umuhimu wa kutumia Rasilimali za Bara la Afrika kwa Ufanisi ili Kuchochea Maendeleo,” yaliyoandaliwa katika Mkutano wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika kwenye Hoteli ya Sofitel Ivoire jijini Abidjan.
Ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa miundombinu katika mageuzi ya kiuchumi, Serikali ya Tanzania imeimarisha juhudi za ndani kufadhili miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na barabara kuu zinazounganisha mataifa mbalimbali kwa lengo la kurahisisha biashara na usafirishaji.
Makamu wa Rais ametaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kama vile kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kielektroniki, kuanzisha Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya Walipa Kodi, pamoja na kukuza soko la mitaji kwa kupitia utoaji wa hatifungani.
Vilevile, amebainisha mchango wa mifuko ya hifadhi ya jamii katika ujenzi wa barabara na madaraja, pamoja na matumizi ya mikopo nafuu kutoka kwa mashirika ya fedha ya kimataifa na nchi marafiki katika kufanikisha miradi hiyo.
Aidha, Dkt. Mpango ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Rais wake anayemaliza muda wake, Dkt. Akinwumi Adesina, kwa ushirikiano wao na Tanzania, hasa katika kusaidia ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na reli ya SGR inayoelekea Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika sekta ya nishati, Makamu wa Rais amesema Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa, ikiwemo kukamilika kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere linalozalisha megawati 2,115, pamoja na uwekezaji katika gesi asilia na nishati ya jotoardhi, ambapo megawati 500 zinatarajiwa kuzalishwa.











