WANAHARAKATI WATOA RAI KWA WANAOCHOCHEA VURUGU NCHINI
Dar es Salaam – Baadhi ya wanaharakati nchini Tanzania wametoa wito kwa vijana kutoka nchi jirani ya Kenya kuacha vitendo vya kumkebehi na kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na kuchochea vurugu na uchochezi ndani ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwanaharakati Ahmedi Kombo alisema kuwa vitendo hivyo vinaharibu taswira ya taifa na viongozi wake, wakati ambapo Rais Samia anaendelea na juhudi za kuleta maendeleo na kuinua uchumi wa nchi.
“Sisi kama vijana wazalendo tumeona ni vyema kutoa tamko kuhusu yanayoendelea. Hatutakubali mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi yetu. Vilevile, mwanasiasa kutoka Kenya, Martha Karua, anapaswa kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi yetu na kumuacha Rais wetu aendelee na kazi za maendeleo,” alisema Kombo.
Kombo aliongeza kuwa taifa liko salama na linaelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa utulivu, huku vyombo vya dola vikiendelea kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Kwa upande wake, mwanaharakati Joseph Yona alieleza kuwa baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikihusika na uchochezi kupitia watu wachache, hali inayochafua taswira ya viongozi wa taifa.
“Nchi yetu ina amani, lakini kuna watu wachache, akiwemo Maria Sarungi na kundi lake, wanaotaka kuigeuza Tanzania kuwa uwanja wa mapambano. Tunasisitiza kuwa Tanzania haihitaji vita wala vurugu – tunahitaji amani,” alisema Yona.
Wanaharakati hao pia walieleza wasiwasi wao kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, wakisema yanachangia kusambaza taarifa potofu na kuchochea taharuki. Wamesisitiza umuhimu wa kulinda heshima ya viongozi na taifa kwa ujumla.





