DKT. MPANGO ASHIRIKI UFUNGUZI WA MKUTANO WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU BAHARI (UNOC3) UFARANSA
Nice, Ufaransa – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3) unaofanyika jijini Nice, nchini Ufaransa.
Mkutano huu wa kimataifa unawaleta pamoja viongozi wa mataifa mbalimbali, wataalamu, wanaharakati wa mazingira na wadau kutoka sekta mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kulinda na kuhifadhi mazingira ya baharini, pamoja na kuendeleza matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika hafla ya ufunguzi, Mheshimiwa Dkt. Mpango alieleza dhamira ya Tanzania katika kuhakikisha uhifadhi wa mazingira ya baharini na kuhimiza ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa bahari na uvuvi haramu.
UNOC3 ni jukwaa muhimu kwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan lengo la 14 (SDG 14) linalolenga kuhifadhi maisha chini ya maji.
Mkutano huu unatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa huku Tanzania ikitarajiwa kutoa mchango muhimu katika mijadala na maazimio yatakayowekwa kwa ajili ya kulinda bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.







