Breaking News

KUMBUKIZI YA KIFO CHA IMAM KHOMEIN, VIJANA WATAKIWA KUILINDA NA KUENZI AMANI

Dar es Salaam – Katika kuadhimisha siku ya kumbukizi ya kifo cha Imam Ruhollah Khomein, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hafla maalum imefanyika katika Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania, ambapo vijana kutoka makundi mbalimbali wameunganishwa na kuhamasishwa kuilinda amani kama tunu muhimu ya Taifa na msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mhe. Emma Nyerere — mwanaharakati wa haki za wanawake, masuala ya kibinadamu na mpigania umoja wa Afrika (Pan-Africanist) — ametoa wito kwa jamii kuepuka mpasuko, ubaguzi na kujiona bora kuliko wengine, akisisitiza kuwa umoja ni msingi wa amani na maendeleo.
"Tusiruhusu mpasuko, wala kujenga matabaka ya huyu kujiona ni bora kuliko mwingine. Palipo na utabaka hapana umoja. Umoja ni chombo pekee kinacholeta amani pia ni nguvu," alisema Mhe. Emma Nyerere.

Akiwakumbusha vijana juu ya umuhimu wa kuzingatia kiasi katika kila jambo, Mhe. Nyerere alimnukuu Imam Khomein akisema kuwa "ukifanya jambo likapita kiasi, amani itatoweka," na kuongeza kuwa: "Moderation is the key to remove division. Kiasi ni ufunguo wa kuondosha matabaka."
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania, Dkt. Mohsen Maarefi, aliwahimiza vijana kuendeleza urithi wa amani uliowekwa na waasisi wa mataifa ya Tanzania na Iran. Alisisitiza kuwa kizazi cha sasa kina wajibu wa kuendeleza mshikamano na kulinda tunu ya amani kama msingi wa kujenga jamii bora.

Maadhimisho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kuenzi mchango wa Imam Ruhollah Khomein na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuhimiza haki, umoja na amani duniani. Vijana wamekumbushwa kuwa nguzo kuu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kitaifa.