Breaking News

SHEIKH PONDA ATOA WITO KWA WATANZANIA KUUNGA MKONO OPERESHENI YA LINDA DEMOKRASIA

Dar es Salaam — Mwenyekiti wa shura ya Imam Tanzania Shiikh ponda Issa Ponda amewataa Watanzania kuungana katika Operesheni ya ACT Wazalendo ya Linda Demokrasia. Operesheni hiyo inalenga kudai haki, kuhakikisha uwazi wa uchaguzi, na kusimamia usawa katika utawala wa nchi.

Akizungumza katika ukaribisho rasmi wa kujiunga na chama cha ACT Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema amani ya kweli haiwezi kujengwa juu ya msingi wa udanganyifu wa kura, ukandamizaji wa sauti za wananchi, na matumizi ya sheria kuwanyamazisha wanaodai haki.

“Taifa letu linahitaji kuongozwa kwa misingi ya sheria – ambapo kila mmoja, bila kujali dini, kabila au nafasi yake katika jamii, anawajibika mbele ya sheria. Sheria inapaswa kulinda haki, siyo kuumiza wananchi,” amesema sheikh Ponda.


Aibua Matukio ya Ukiukwaji wa Haki

Akitaja matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki nchini, ameelezea masikitiko yake juu ya hali inayoendelea kushuhudiwa:
Raia kupigwa kwa sababu ya kutetea kura zao.

Wananchi kuvamiwa kwa kuhudhuria kesi za viongozi wao.

Viongozi wa dini kuwekwa magerezani kwa zaidi ya miaka 10 bila kesi kusikilizwa.

Nyumba za ibada kufungwa na kuvamiwa na vyombo vya dola.

Watu kutekwa na kuuliwa na watu wasiojulikana huku serikali ikikaa kimya.

Aeleza Changamoto za Muundo wa Muungano

Katika hatua nyingine, amegusia muundo wa sasa wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, akisema kuwa mkataba wa mwaka 1964 umetafsiriwa vibaya na kupelekea kutoweka kwa serikali ya Tanganyika ndani ya mfumo wa sasa

“Leo tuna serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar, lakini serikali ya Tanganyika haipo wazi – jambo ambalo linaleta mkanganyiko mkubwa hata katika uongozi wa nchi,” alisema Sheikh Ponda

Amependekeza kuwa kurejeshwa kwa serikali ya Tanganyika na kupatikana kwa Katiba Mpya ni hatua muhimu katika kurekebisha mfumo wa taifa na kuhakikisha kuwa kila upande wa Muungano unatendewa haki.

Atoa Sababu ya Kujiunga na Siasa

Mwanaharakati huyo pia ametangaza kuwa moja ya sababu kuu za kuchukua kadi ya chama cha siasa ni kupata jukwaa la kisheria kuwaelimisha wananchi kuhusu Katiba Mpya na kuwahamasisha kudai mabadiliko ya kweli.
“Mapambano haya si ya mtu mmoja, chama kimoja wala kikundi fulani. Ni mapambano ya kila Mtanzania mpenda haki, amani na maendeleo ya kweli,” alisisitiza.

Viongozi wa Dini Wahimizwa Kuingia Katika Siasa

Katika hitimisho la hotuba yake, alieleza umuhimu wa viongozi wa dini kushiriki katika siasa ili kusaidia kulinda maadili ya taifa na kupambana na ufisadi unaoendelea serikalini.

 “Uwepo wa viongozi wa dini katika vyombo vya maamuzi utasaidia kulinda utu, kuimarisha maadili na kuziba mianya ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka,” alisema. Sheikh Ponda