Breaking News

SHEIKH PONDA AJIUNGA RASMI NA ACT WAZALENDO ASISITIZA "UZALENDO WA KWELI NI KUPINGA DHULUMA "

Dar es Salaam – Sheikh Ponda Issa Ponda amejiunga rasmi na chama cha ACT Wazalendo, akisisitiza umuhimu wa kudai utawala wa sheria, uchaguzi huru na haki kwa taifa la Tanzania.

Akihutubia hadhara ya wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo, Sheikh Ponda amesema ameamua kuchangia nguvu katika Operesheni ya Linda Demokrasia inayoendeshwa na ACT Wazalendo, yenye lengo la kurejesha haki, uwazi na usawa katika michakato ya uchaguzi nchini.

“Natoa wito kwa vijana, wanawake, wazee na viongozi wa dini kuungana katika mapambano ya kudai haki mbalimbali, hususan kuhakikisha kura zinahesabiwa kwa haki na viongozi wanaochaguliwa wanawakilisha matakwa ya wananchi,” alisema Sheikh Ponda.
Alisisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana endapo kura zinaibiwa na sauti za wananchi zinakandamizwa, akionya dhidi ya matumizi mabaya ya sheria kama vile ile ya Kupambana na Ugaidi kuwanyamazisha wakosoaji wa mfumo wa sasa wa utawala.

Katika hotuba yake, Sheikh Ponda alilaani vitendo vya ukatili dhidi ya raia, wakiwemo viongozi wa dini wanaowekwa magerezani kwa miaka mingi bila kuhukumiwa, nyumba za ibada kufungwa, na wananchi kutekwa na kuuawa bila ulinzi wa dola.

Akiangazia masuala ya kikatiba, Sheikh Ponda alisema kuwa mfumo wa Muungano uliopo sasa umeathiri sana uwiano wa mamlaka baina ya Tanganyika na Zanzibar, akisema Tanganyika imefichwa na Muungano umechakachuliwa kwa kubadili Katiba mara kwa mara. Alitoa mfano kuwa Zanzibar ina serikali na Rais wake, huku Tanganyika ikiwa haina uwakilishi wa moja kwa moja kama taifa.