TANZANIA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA DENMARK, YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameongoza Watanzania na Wanadiplomasia katika maadhimisho ya Siku ya Katiba ya Denmark yaliyofanyika katika makazi ya Balozi wa nchi hiyo, jijini Dar es Salaam tarehe 05 Juni, 2025.
Siku ya Katiba ya Denmark, huadhimishwa tarehe 5 Juni kila mwaka kukumbuka kupitishwa kwa katiba ya kwanza ya kidemokrasia ya Denmark mwaka 1849 na huheshimiwa kama siku ya Kidemokrasia ya Taifa hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kombo alitoa salamu za pongezi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, na wananchi wa Tanzania kwa Mheshimiwa Mfalme Frederik X, wa Denmark na raia wake, kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa uwili kati ya Tanzania na Denmark.
“Denmark ilikuwa nchi ya kwanza kuingia makubaliano ya misaada ya maendeleo na Tanzania baada ya kutunga sheria yake ya maendeleo ya kimataifa, hatua iliyoanzisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizi mbili, ambao umeendelea kukua katika maeneo ya utawala wa uchumi, afya, na maendeleo ya sekta binafsi,” alifafanua Mhe. Kombo.
Ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Denmark kuongeza uwekezaji wao katika sekta za afya, kilimo, viwanda, utalii, na nishati safi, pamoja na kujenga ofisi zao jijini Dodoma ili kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania .
Awali, Balozi wa Denmark nchini, Mhe.Jesper Kammersgaard, aliipongeza Tanzania kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika nyanja za kiuchumi, miundombinu na maendeleo ya kijamii na kuongeza kuwa mafanikio hayo yameihamasisha Denmark kuendelea kuimarisha uhusiano wake wa kirafiki na kindugu na Tanzania.


.jpg)






