Breaking News

WAZIRI KOMBO APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA BALOZI MTEULE WA ALGERIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya watu wa Algeria Mheshimiwa Balozi Zermane Ghalib, katika hafla iliyofanyika tarehe 5 Juni, 2025 kwenye Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kupokea Nakala za Hati hizo, Balozi Kombo amesema uhusiano kati ya Tanzania na Algeria umejengwa katika misingi ya kihistoria tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na umeendelea kuimarika kupitia ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii.
AmesemaTanzania na Algeria zinataendelea kuimarisha ushirikiano wa uwili katika biashara ikiwemo mazao ya kilimo, bidhaa za viwandani, nishati na gesi asilia, madini, nishati, utalii na uchumi wa buluu.

Waziri Kombo amempongeza Mhe. Ghalib kwa uteuzi wake na kumhakikishia ushirikiano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikalini kwa ujumla; kwa kipindi chote atakachohudumu hapa nchini.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Ghalib, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kueleza dhamira ya nchi yake ya kuhamasisha sekta binafsi ya Algeria kuja kuwekeza nchini pamoja na kufungua fursa za bidhaa za Tanzania kuingia katika soko la Algeria kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi ya mataifa yote mawili.

Mheshimiwa Ghalib pia ameeleza kuwa serikali ya Algeria iko tayari kushirikiana na Tanzania kuanzisha miradi ya pamoja, hasa kupitia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (African Continental Free Trade Area -AfCFTA), ili kukuza biashara kati ya nchi za Afrika.