Breaking News

WAZIRI KOMBO AKABIDHI HATI YA KIWANJA KWA UBALOZI WA OMAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo amemkabidhi Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saudi Al Hilal Shidhani, Hati ya Kiwanja kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi huo jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kukabidhi Hati hiyo ya Kiwanja katika hafla iliyofanyika tarehe 05 Juni,2025 katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri Kombo aliishukuru Serikali ya Oman kwa uamuzi wa kujenga Kituo cha Utamaduni cha Oman, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman.
Alisisitiza kuwa kuwa kituo hicho hakitakuwa tu mahali pa kuhifadhi na kuendeleza utamaduni, bali pia kitakuwa kivutio kwa wanataaluma, watafiti, na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kusaidia kuongeza mapato ya utalii na kuchangia kukuza uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini Mhe. Saudi al Hilal Shidhani, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kiwanja hicho ambacho kitakachotumika kujengea kituo kinachotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kiutamaduni kati ya Tanzania na Oman, wenye historia ndefu ya kijamii na kiuchumi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule; Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.