Breaking News

POLISI DAR ES SALAAM YATOA TAARIFA YA HALI YA USALAMA NA MAFANIKIO YA HUKUMU YA KESI ZILIZOFIKISHWA MAHAKAMANI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia na kupambana na vitendo vya kihalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza mapema leo jijini dar es salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Jumanne Muliro amesema hali ya usalama kwa ujumla ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida.

Kamanda Murilo aliongeza kuwa katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Novemba 2025, Jeshi la Polisi limefanikiwa kufikisha mashauri mbalimbali katika Ofisi ya Mashitaka na baadaye Mahakamani, ambapo baadhi ya watuhumiwa waliokutwa na hatia wamehukumiwa adhabu kali, hususan kwa makosa yanayohusiana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Miongoni mwa waliopatikana na hatia ni pamoja na Abubakari Memba maarufu kwa jina la Abuu, mkazi wa Mbagala, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la kulawiti. Julius Jasto maarufu Mbwambo, mkazi wa Ukonga, naye alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa hilo hilo.

Aidha, Paul Elisha mkazi wa Kawe alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa kosa la kubaka, huku Erick Muhagama mkazi wa Kimara akihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kwa kosa la kulawiti.

Kwa upande wa makosa mengine, Khalifani Ramadhani mkazi wa Kiponza, Chamazi, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Vilevile, Jackson Tumwesige na Abrahamani Hassani maarufu Mkwawa, wakazi wa Ukonga, walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali.

Katika kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema litaendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi pamoja na nyumba za ibada ili kubaini, kuzuia na kutanzua matukio ya kihalifu kabla, wakati na baada ya sherehe hizo.

Jeshi la Polisi limewataka wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wao wakati wa matembezi na mikusanyiko mbalimbali, huku likisisitiza nyumba na makazi yasiachwe bila uangalizi. Aidha, ukaguzi wa kushitukiza wa usalama barabarani pamoja na upimaji wa madereva wa vyombo vya moto umeanza, na watumiaji wote wa barabara wametakiwa kuzingatia sheria ili kuepusha ajali.

Kamanda huyo ameonya kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali na za haraka za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuvunja sheria. Vilevile, wananchi wameonywa dhidi ya matumizi ya baruti au fataki bila vibali vya kisheria, kwani vitendo hivyo husababisha usumbufu na hofu kwa umma.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatakia wananchi maandalizi mema ya sikukuu hizo na kuhimiza kusherehekea kwa amani na usalama.