TANESCO YATOA TAARIFA KUHUSU MABORESHO YA KITUO CHA KUPOKEA NA KUPOZA UMEME CHA NYAKATO – MWANZA
Mwanza - Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawaarifu wateja wake wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani kuwa limekamilisha kazi za maboresho ya Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Nyakato, licha ya changamoto iliyosababisha kuchelewa kurejea kwa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo.
Awali, TANESCO ilikuwa imepanga kutekeleza katizo la umeme siku ya Jumapili, tarehe 21 Desemba 2025, kuanzia saa 02:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni, ili kuruhusu utekelezaji wa kazi hizo muhimu za maboresho. Hata hivyo, mvua kubwa iliyonyesha nyakati za asubuhi ilisababisha kazi kushindwa kuanza kwa wakati uliopangwa.
Kutokana na hali hiyo, utekelezaji wa kazi ulianza saa 06:00 mchana na kukamilika saa 05:00 usiku, hali iliyopelekea huduma ya umeme kuchelewa kurejea kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Maboresho haya ni sehemu ya mpango endelevu wa TANESCO wa kuimarisha miundombinu ya umeme ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika katika Jiji la Mwanza na maeneo ya jirani, sambamba na kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.
TANESCO itaendelea kuwataarifu wateja wake mapema kuhusu maboresho mengine yatakayopangwa kutekelezwa siku zijazo.
Shirika linaomba radhi kwa usumbufu uliowapata wateja wake kutokana na kuchelewa kurejea kwa huduma ya umeme na linawashukuru kwa uvumilivu na ushirikiano wao wakati wa utekelezaji wa kazi hizi muhimu za maendeleo.









