ACT WAZALENDO WAITAKA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA KALI WATUHUMIWA WA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA UMMA
Dar es Salaam - Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuwafikisha mahakamani watumishi na viongozi waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uchambuzi wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema kuwa licha ya ripoti za CAG kuendelea kubainisha mianya ya ubadhirifu kila mwaka, hatua madhubuti dhidi ya wahusika zimekuwa hazichukuliwi.
Alieleza kuwa ripoti ya mwaka 2024/2025 imeonesha ongezeko kubwa la fedha zilizopotea, zikifikia takribani shilingi trilioni 7, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.5 zilizoripotiwa katika mwaka wa fedha 2023/2024.
“Kila mwaka ripoti ya CAG inaonesha upotevu mkubwa wa fedha za umma, lakini wahusika hawaadhibiwi ipasavyo. Hali hii inachochea kuendelea kwa ubadhirifu nchini,” alisema Shaibu.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua hatua kali, ikiwemo kuwafikisha mahakamani wote waliotajwa katika ripoti hiyo ili kurejesha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Aidha, Shaibu aliwataka wananchi kutumia ripoti za CAG kama nyenzo ya kuwawajibisha viongozi, kwa kuwahoji na kudai uwajibikaji pale inapobainika kuwepo kwa matumizi mabaya ya rasilimali za taifa.
Deni la Taifa Latia Wasiwasi
Akizungumzia hali ya uchumi, Shaibu alisema deni la taifa limefikia takribani shilingi trilioni 110, likiongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni 12.7. Alidai kuwa kiwango hicho ni mzigo mkubwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa maelezo yake, mgawanyo wa deni hilo kwa idadi ya wananchi unaashiria kuwa kila Mtanzania anabeba mzigo wa takribani shilingi milioni 1.8.
“Hili ni deni kubwa linaloweza kuwaathiri wananchi moja kwa moja kupitia kodi na gharama za maisha,” alionya.
Wito wa Mageuzi Sekta ya Nishati
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita, aliitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za kupanda kwa bei ya mafuta duniani, hususan kutokana na mvutano wa kisiasa katika Mashariki ya Kati.
Alipendekeza matumizi ya nishati mbadala, ikiwemo gesi asilia, katika vyombo vya usafiri kama magari, bajaji na pikipiki ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli.
Changamoto Sekta ya Afya
Naye kiongozi wa chama hicho, Doroth Semu, alisema ripoti ya CAG imebainisha kuwa Bohari ya Dawa (MSD) inaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 47.11.
Alisema hali hiyo inaathiri upatikanaji wa dawa kwa wakati, na kuitaka Serikali kulipa deni hilo haraka ili kuhakikisha huduma za afya zinaimarika.
Katika hatua nyingine viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa viongozi wa umma, usimamizi madhubuti wa rasilimali za taifa, pamoja na utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya CAG ili kudhibiti ubadhirifu na kuimarisha uchumi wa nchi.




