Breaking News

AMANI NA UWAJIBIKAJI WA WANANCHI: NGUZO YA MAENDELEO YA TAIFA - MWENEZI KENANI

Geita — Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Kenani Kihongosi, amewahimiza Watanzania kuachana na mikumbo ya malumbano yasiyo na tija na badala yake kujikita katika kulinda amani na kuchochea maendeleo ya jamii.

Akizungumza na wananchi wa Katoro mkoani Geita, Kihongosi alisisitiza kuwa maendeleo ya maeneo wanayoishi wananchi yako mikononi mwao wenyewe, huku akieleza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa ustawi wa kijamii na kiuchumi.

“Maendeleo ya eneo mnaloishi yapo mikononi mwenu na amani ndiyo msingi mkuu wa ustawi wenu,” alisema.

Alifafanua kuwa uwepo wa mikutano ya kisiasa pamoja na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo unatokana na hali ya utulivu na amani iliyopo nchini, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuilinda.

Kihongosi alionya kuwa vurugu na migogoro isiyo na tija husababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na upotevu wa mali, kuhatarisha usalama wa raia na kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.

Aidha, aliwataka wananchi, hususan vijana, kuwa makini dhidi ya ushawishi wa watu au makundi yenye nia ya kuvuruga amani kwa maslahi yao binafsi. Alibainisha kuwa mara nyingi wachochezi wa vurugu hawapati madhara ya moja kwa moja, bali waathirika wakubwa huwa ni wananchi wa kawaida.

Katika hatua nyingine, aliwahimiza vijana kuelekeza nguvu zao katika shughuli halali za kiuchumi kama vile biashara, kilimo na ufugaji ili kujipatia kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.

Wito huo unakuja katika kipindi ambacho juhudi za kuimarisha mshikamano wa kitaifa na maendeleo endelevu zinaendelea kupewa kipaumbele nchini.