Breaking News

MARIDHIANO UPONYA MAJERAHA - JAJI CHANDE

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mohamed Chande Othman, amesema vurugu zilizotokea zimeacha nyufa na majeraha kwa taifa, hivyo maridhiano ni hatua muhimu katika kuponya majeraha na kurejesha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Jaji Chande ameeleza kuwa suala la maridhiano halikuanza baada ya ghasia, bali lilianza kuzungumzwa kwa maoni ya wengi tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani.

Amesema kuna umuhimu wa kufanya majadiliano baina ya dini kama sehemu ya mchakato wa maridhiano ya kijamii, ambayo yatasaidia kuleta maelewano miongoni mwa viongozi wa dini pamoja na kuweka mipaka kati ya dini na siasa.

Aidha, amependekeza kuwa maoni na mapendekezo yatokanayo na majadiliano hayo yapelekwe serikalini ili kusaidia kuepuka migongano katika siku zijazo.

Jaji Chande amependekeza pia kuwa maridhiano katika ngazi ya kitaifa yashuke hadi ngazi za serikali za mitaa kupitia mifumo ya utawala iliyopo.

Vilevile, amependekeza kuanzishwa kwa baraza la ushauri la wazee litakalosaidia kutoa ushauri na kupunguza mivutano katika jamii pamoja na masuala mengine ya kitaifa.

Jaji Chande ameyasema hayo leo Aprili 23, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi ripoti ya Tume hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.