Breaking News

VIJANA WAKUMBUSHWA WAJIBU WA KULINDA AMANI NA UMOJA WA TAIFA

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Salum Gumbo, ametoa wito kwa vijana nchini kulinda na kudumisha amani, akisisitiza kuwa wao ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Youth Platform) pamoja na Kongamano la Vijana, Gumbo alisema mustakabali wa taifa hasa katika masuala ya amani, umoja na mshikamano upo mikononi mwa vijana. Alieleza kuwa kundi hilo lina jukumu kubwa la kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu na yenye mshikamano.

“Vijana msichukulie kwa mzaha wajibu wenu katika ujenzi wa taifa. Ninyi ndio nguvu kazi na uti wa mgongo wa maendeleo ya sasa na ya baadaye,” alisema Gumbo.

Aidha, aliwahimiza vijana kujifunza na kuielewa historia ya Tanzania ili kujikinga dhidi ya upotoshaji unaoweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa. Alionya kuwa mara nyingi maadui wa taifa huanza kwa kupotosha historia ili kudhoofisha misingi ya umoja na uzalendo.

Kwa upande wake, alibainisha kuwa majukwaa kama hayo ya vijana ni fursa muhimu ya kujenga uelewa, kubadilishana mawazo, na kuimarisha ushiriki wa vijana katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kongamano hilo limekusanya vijana kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kujadili nafasi yao katika maendeleo ya taifa, huku likitoa msisitizo wa maadili, uzalendo na uwajibikaji kama nguzo za mafanikio ya kizazi cha sasa na kijacho.