ACT WAZALENDO YAJADILI HALI YA KISIASA NCHINI, OTHMAN MASOUD OTHMAN ATOA WITO WA MAELEKEO MPYA KWA TAIFA
Dar es salaam - Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Mhe. Othman Masoud Othman, leo Mei 03 2026, ameshiriki na kuongoza Kikao cha Kamati Kuu Maalum ya Chama hicho, huko katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema, uliopo ndani ya Jengo la Maalim Seif, Makao Makuu ya ACT Wazalendo, Magomeni Jijini Dar es Salaam.
Akitoa salamu zake wakati wa Ufunguzi wa Kikao hicho cha Dharura, kinacholenga kujadili hali ya kisiasa Nchini, Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa Viongozi wa ACT Wazalendo kutumia hekima na uweledi mkubwa walionao, ili kusaidia namna ya kuwafikisha Watanzania katika Mafanikio, baada ya kukatishwa tamaa kwa muda mrefu, kufuatia tawala zisizojali Maslahi ya Taifa.
Amesema, "hii ni kutokana na ukweli wa dhati kwamba wale waliojipa Mamlaka ya Kuliongoza Taifa hili wanatukosea sana kwa kushindwa kusimamia Misingi ya Haki, Uadilifu na Ustaarabu"
Amefahamisha kuwa wanachohitaji Watanzania na Matumaini makubwa mbele ya Viongozi wa Chama hicho ni kutengeneza 'barabara' itakayowafikisha katika matarajio yao.
"Give your emotions, all the intellects you have...", amekariri maneno hayo yanayolenga haja ya kuchunga maono, ili kulinda hadhi, heshima, hikma na uelewa, ili kusaidia matarajio ya wananchi katika kuwaletea maendeleo; akisisitiza kuwa hiyo ndiyo haja ya kila Kiongozi wa Watu, hasa ndani ya ACT Wazalendo.
"Naamini wengi wamevunjika moyo, wakiwa wamekata tamaa, wakiamini mwelekeo wa sasa hauakisi yale Machozi na Machungu waliyonayo, kutokana na matukio ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana yaliyotokea; hebu tuwatengenezee Watanzania, barabara safi ya kuyafikia mafanikio ya kweli na matarajio yao", amesisitiza usoni mwa Wajumbe wa Kikao hicho.
Aidha ameongeza kwa kusema, "tunahitaji kuziendea Ajenda tutakazozizungumza kwa umakini wa hali ya juu; hatuhitaji kuangalia nani katenda nini, bali tuangalie ukubwa wa Taifa letu, hasa Tanzania yetu bora inavyozungumzwa na Majirani".
"Tuitizame Nchi yetu, na Taasisi zake Madhubuti; tuyazingatie hayo sambamba na kujali matarajio na matumaini makubwa kwetu kutoka kwa Umma uliokwishakatishwa tamaa", ameongeza.
Akifungua Kikao hicho ametangulia-kusema, "napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia tukafika katika Kikao hiki Maalum Muhimu kwaajili ya Mustakbala mwema wa Nchi na Taifa letu".
Akitoa maelezo ya Utangulizi, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ndugu Ado Shaib (Mb) amekitaja Kikao hicho kuwa ni cha Dharura, kikiwahusisha pia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, pamoja Wabunge wa Bunge la Jamhuri, ambao kwa upande wao ni Waalikwa.
Kikao hicho kilitanguliwa na Kikao cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika mnamo Aprili 29 Mwaka huu, katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Vuga Mjini Unguja na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Kiongozi wa Chama, Bi. Doroth Semu.
Aidha, Kikao hicho kinatarajiwa kutoka na Maazimio ya Msimamo wa Chama, kufuatia kile kilichotajwa ni mwenendo wa sasa unaogusa mambo mbali mbali ya kisiasa Nchini.
Viongozi Wakuu na Watendaji mbalimbali wa ACT Wazalendo Taifa, wamehudhuria hapo, wakiwemo Makamu Wenyeviti wa Chama hicho Tanzania Bara na Zanzibar, Ndugu Is-haka Mchinjita, na Ndugu Ismail Jussa.








