RAIS SAMIA AMTUNUKU PROFESA NDUNGURU TUZO YA MFANYAKAZI HODARI KWA MAGEUZI MAKUBWA TPHPA
Mwandishi Wetu, Njombe - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, juzi Mei 1 katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa, alimkabidhi tuzo ya Mfanyakazi Hodari, cheti na zawadi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Joseph Ndunguru.
Profesa Ndunguru, ambaye anatoka katika Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi za utafiti (RAAWU), alijiunga na TPHPA mwaka 2023. Tangu hapo, ameiongoza taasisi hiyo kufanya mageuzi makubwa yaliyoiwezesha kuwa mfano barani Afrika.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa uwezo wa uchambuzi wa viuatilifu, kuboreshwa kwa maabara hadi kufikia viwango vya kisasa, pamoja na kuunganisha ofisi 47 zilizopo mipakani mwa Tanzania katika mfumo mmoja wa kidijitali unaorahisisha utendaji kazi. Maboresho hayo yameongeza ufanisi na mapato ya taasisi hiyo kutoka shilingi bilioni 14 mwaka 2023 hadi kufikia bilioni 69 ndani ya miezi minane tu kuanzia Julai 2025 hadi Februari mwaka huu.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Samia aliwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa mchango wao katika kukuza uchumi wa taifa, akiahidi kuendelea kuboresha maslahi yao.
“Chapeni kazi, Serikali inatambua mchango wenu. Kadri hali ya uchumi inavyozidi kuimarika, tutaendelea kuboresha maslahi yenu. Pia tunaendelea kulipa madai yenu na kutafuta fursa zaidi za ajira zenye staha ndani na nje ya nchi,” alisema.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Profesa Ndunguru alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya TPHPA na Serikali, pamoja na mshikamano wa wafanyakazi wa mamlaka hiyo katika kutekeleza maelekezo ya Rais.
“Ushindi huu si wangu peke yangu, bali ni wa wafanyakazi wote wa TPHPA. Tumefanikiwa kwa pamoja, na leo tunapokea watafiti na wanasayansi kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujifunza kutoka kwetu,” alisema.
Aliongeza kuwa maboresho ya maabara nchini yameondoa ulazima wa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo kwenda nje ya nchi kupima ubora wa bidhaa zao kwa ajili ya masoko ya kimataifa.
“Zamani tulipeleka mazao kupimwa nje, lakini sasa tuna uwezo wa kufanya vipimo hapa hapa nchini, na maabara zetu zinatambulika kimataifa,” alisisitiza.
Kuhusu mchango kwa wakulima, alisema TPHPA imekuwa ikisaidia kuzalisha mazao bora na salama, pamoja na kutafuta masoko ya kimataifa, hasa kwa mazao ya kimkakati.
Alibainisha kuwa kampuni 16 zinazojihusisha na mazao ya parachichi na viazi mviringo zimewezeshwa kupata masoko nchini China, huku wakulima wadogo wakisaidiwa kusafisha mazao yao kabla ya kusafirishwa nje.
Aidha, alisema ujenzi wa maabara mpya unaendelea katika makao makuu ya TPHPA mkoani Arusha na Makambako, pamoja na mpango wa kujenga ghala la kuhifadhi mbegu za asili 10,000 kwa ajili ya matumizi ya wakulima na watafiti.
Kwa sasa, TPHPA ina uwezo wa kuchambua sampuli 2,000 kwa wiki, hatua inayopunguza ucheleweshaji wa utoaji wa ithibati kwa matumizi mbalimbali.
Profesa Ndunguru pia aliahidi kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari (JOWUTA) kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu shughuli za mamlaka hiyo, pamoja na kusaidia kufichua matumizi ya viuatilifu visivyoidhinishwa ili kulinda afya ya binadamu na mimea.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma, alimpongeza Profesa Ndunguru na wafanyakazi wote wa TPHPA kwa kazi nzuri wanayofanya, huku akiishukuru taasisi hiyo kwa kuwa mdhamini wa tuzo za wanahabari hodari mwaka 2026.tq7o






