UJUMBE WA TANZANIA WASHIRIKI MKUTANO WA KIMKAKATI WA USIMAMIZI WA MAAFA ZIMBABWE
MASVINGO, ZIMBABWE – Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Usimamizi wa Maafa wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika mjini Masvingo, Zimbabwe. Mhe. Mmuya anamwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Profesa Palamagamba Kabudi.
Mkutano huo umejadili maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa programu za kikanda pamoja na masuala ya kimkakati yanayohusu usimamizi wa maafa katika nchi za SADC. Aidha, jukwaa hilo limetumika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, washirika wa maendeleo wa kimataifa na jumuiya ya wafadhili kwa lengo la kuongeza uwekezaji katika sekta ya usimamizi wa maafa na kujenga ustahimilivu wa kikanda.
Katika ujumbe huo, Mhe. Mmuya ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. CP Suzan Kaganda; Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi; Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala; pamoja na viongozi na maafisa mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.







