WAZIRI SANGU AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI KUIMARISHA MSHIKAMANO WA KITAIFA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amekutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Kanisa la Gospel Revival Centre (GRC), Mchungaji Antony Lusekeleo anayefahamika zaidi kwa jina la Mzee wa Upako sambamba na kiongozi wa kiroho wa kanisa la King Dom Embassy, Crear Malisa.
Mazungumzo ya watatu hao waliokutana jijini Dar es Salaam yalijikita katika kuimarisha na kuboresha ushirikiano wa Serikali na taasisi za dini kwenye kukuza ustawi wa jamii na mshikamano wa kitaifa.
“Serikali ya Awamu ya Sita ilianzisha Idara maalumu ya Mahusiano chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuimarisha uratibu wa masuala ya kijamii na kitaasisi, ikiwemo mahusiano ya kazi, mahusiano kati ya serikali na wadau wa kijamii, vyama vya siasa na taasisi za dini sambamba na kuimarisha amani, umoja na mshikamano katika jamii.” Amesema Waziri Sangu na kuongeza kuwa
“Mshikamano wa kijamii na maadili ni nguzo muhimu katika kulinda amani na utulivu wa taifa na viongozi wa dini ni mhimili wa kujenga mshikamano wa kijamii na kulea wafuasi kwa maadili yanayompendeza Mungu ambayo yanahimiza na kusisitiza amani na mshikamano miongoni mwa wanajamii”.
Kwa upande wao, viongozi hao, Mchungaji Antony Thomas Lusekeleo ‘Mzee wa Upako’ na Crear Malisa wa King Dom Embassy Church wameipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele katika masuala ya mahusiano ya Serikali na makundi mbalimbali na kueleza utayari wa kushirikiana na serikali katika kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza maadili ya taifa.




